Muuguzi anayedaiwa kumwambia mama wa mgonjwa ‘ataisoma namba kumchagua Magufuli’ atambuliwa


Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Gloria Mbwille alisema muuguzi huyo ametambuliwa na kwamba tume imeundwa kuchunguza tuhuma zinazomkabili.

Hata hivyo, alikataa kuzungumzia zaidi kuhusu muuguzi huyo wala kumtaja jina akisema taarifa zaidi zitatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla baada ya tume kukamilisha uchunguzi huo. Juzi mchana, Junes alimueleza Makalla kwamba alifika hospitalini hapo Novemba 22 asubuhi akitokea wilayani Mbozi.

Alisema baada alifuata taratibu za kufungua kadi kwa gharama ya Sh5,000 kwa ajili ya kutaka matibabu ya mtoto wake, Joyce Asifiwe (9), lakini alikashfiwa kwenye dirisha la dawa akiambiwa ataisoma namba kwa kumchagua Rais Magufuli.

Alisema baada ya kumuona daktari aliandikiwa dawa za kwenda kuchukua kwenye dirisha ambako ndiko alikotolewa maneno ya kashfa.

“Kwenye dirisha hilo nilimkuta muuguzi mmoja ambaye aliniambia kwamba dawa zote zinauzwa. Hapa hakuna dawa za bure, si mlimchagua Magufuli, sasa mtaisoma namba,’’ alisema akidai kumnukuu aliyemtaja kuwa ni muuguzi.


Baada ya kumsikiliza malalamiko hayo, Makalla aliagiza mganga mkuu aitwe, lakini ilielezwa alikuwa safarini, hivyo kaimu wake, Dk Ismail Macha alifika.

Makalla alimueleza Dk Macha kwa kifupi yaliyojiri kutoka kwa mlalamikaji huyo na kumtaka waongozane hadi hospitalini na kuwaita wauguzi waliokuwa zamu Novemba 22 dirisha la dawa ili amtambue mhusika na achukuliwe hatua jambo ambalo limefanyika.

No comments:

Post a Comment

Adbox

@templatesyard