MAUAJI
ya watu watatu wa familia moja yaliyotokea jijini Mwanza hivi karibuni
yameibua maswali mengi lakini mwisho wa yote, imebainika kuwa
kilichoiponza familia hiyo kukumbwa na mauti hayo ni hiki, Uwazi
limechimba mwanzo mwisho.
Mauaji
hayo yalitokea saa 10 alfajiri ya Septemba 21, mwaka huu katika Kijiji
cha Ihila, Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza ambapo
inaaminika kuwa mgeni aliyekaribishwa kwenye familia hiyo ndiye
aliyetekeleza mauaji hayo na alikaribishwa nyumbani hapo bila kujulikana
tabia.
Debora
Jonas Luhinga, mtoto wa marehemu ambaye alinusurika katika tukio hilo,
alisema kuwa mgeni huyo aliyemfahamu kwa jina moja la Lameck alifika
nyumbani hapo Septemba 18, mwaka huu lakini baada ya kutekeleza mauaji
hayo alitokomea kusikojulikana.
Debora
mwenye umri wa miaka 12, alidai kuwa siku ya tukio, usiku akiwa
amelala, mdogo wake aitwaye Eliudi aliyekuwa amelala naye aliamka na
kuanza kulia sana.
Alisema
alichukua jukumu la kumbembeleza mdogo wake huyo lakini ilishindikana,
ghafla Lameck aliingia chumbani humo na kumwomba mtoto huyo ili
ampeleke chumbani kwa wazazi wake akabembelezwe.
“Kilio
cha mdogo wangu kilikuwa kikubwa, mara nikaona mlango unafunguliwa,
Lameck akaingia, akasema kwa kuwa mtoto analia sana nimpe ampeleke kwa
mama ili akambembeleze,” alisema Debora.
Akaongeza kuwa alikubali kumpa Lameck mtoto huyo na kwa vile yeye alikuwa na usingizi mzito aliendelea kulala fofofo.
Debora alisema alipoamka kulikuwa kumekucha, akashuka kitandani ili aende nje lakini akakuta mlango umefungwa kwa nje.
“Nilipiga
kelele baada ya kukuta mlango wa chumba changu umefungwa kwa nje,
majirani walifika kunifungulia lakini nilipigwa na mshangao kukuta maiti
ya baba ikiwa sakafuni sebuleni tena imetapakaa damu.
“Nikiwa
nimechanganyikiwa niliingia chumbani kwa wazazi wangu, nikashangaa
kumuona mama yangu na mdogo wangu Eliudi wakiwa wameuawa kwa kunyongwa
na miili yao imelazwa chini,” alisema Debora.
Debora
alisema anaamini Lameck ambaye mara nyingi alikuwa akimwona akizungumza
na baba yake ndiye aliyetenda unyama huo. Alisema anaamini mtu huyo
wakati anaingia chumbani kwake kumchukua mdogo wake alikuwa ameshawaua
wazazi wake na aliamua kumtwaa mtoto huyo kwenda kumnyonga ili kilio
chake kisiwafanye majirani wakafika nyumbani hapo kutaka kujua kulikoni
na hivyo kugundulika alichokifanya kwa muda huo.
Alikwenda mbele zaidi kwa kusema anaamini baba yake ndiye aliyeanza kuchinjwa kabla ya mama yake kunyongwa.
Baadhi
ya majirani waliozungumza na gazeti hili huku wakiomba majina yao
kuhifadhiwa baada ya tukio hilo, walisema kwa nyakati tofauti kuwa
huenda mauaji hayo ni ya kulipiza kisasi kwa mwanaume huyo ila mkewe na
mtoto waliingizwa kwenye mkumbo tu.
Walisema haiwezekani watu wa familia moja wakauawa kikatili namna hiyo bila ya wauaji kuanika sababu.
Waliongeza kwa kudai kuwa siku zote tatu alizoishi hapo, Lameck alikuwa akitafuta njia mwafaka ya kutekeleza ukatili huo.
Walisema
mauaji mengi ya aina hiyo yanayotokea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa
wa Mwanza huhusishwa na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi au
mirathi.
Majirani
hao waliongeza kuwa awali walikuwa wakimwona Lameck nyumbani kwa
marehemu bila kujua uhusiano wao, wakaonya kuwa ni hatari sana
kumkaribisha nyumbani mtu usiyemjua kwa undani kama ilivyokuwa kwa
Lameck.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Ernest Mangu alithibitisha kutokea kwa
mauaji hayo huku akisema hakuna aliyekamatwa. Aliwataja marehemu kuwa ni
Jonas Luhinga, mkewe Rusia Jonas na mtoto wao, Eliud Jonas.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment