KILA MWENYE SIMU KULIPA DENI SH 3000


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekiri kuziandikia waraka kampuni za simu nchini kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini mara moja kuanzia mwezi huu. Kodi hiyo mpya ilipitishwa wakati wa Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kutaka utekelezaji wake uanze Julai 30, ili kusaidia shughuli za bajeti ya Serikali Kuu.
Akijibu swali kuhusu ukweli wa Mamlaka hiyo kuagiza kampuni hizo kuanza rasmi kutoza kodi hiyo mwezi jana, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mteja, Huduma na Mapato wa TRA, Richard Kayombo, alikiri kutoa agizo hilo.
“Sitaki kuzungumzia kiundani sana suala hili, lakini ukweli ni kwamba kampuni hizi za simu zimeandikiwa kuanza kulipa kodi na tumeandika kwa ajili ya utekelezaji wa kodi hii mpya,” alisema Kayombo.
Alisema ingawa kweli kampuni hizo zimeagizwa kuanza kutoza kodi hiyo, hatazungumzia zaidi suala hilo kwa kuwa tayari liko mahakamani hivyo si vema kuingilia uhuru wa mhimili huo. Wakati TRA ikitoa agizo hilo, Taasisi ya Watumiaji wa Bidhaa na Huduma ilifungua kesi Mahakama Kuu kupinga sheria hiyo.
Taasisi hiyo ilifungua kesi hiyo hivi karibuni katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura na kuanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Lawrence Kaduri, Aloysius Mujulizi na Salvatory Bongole.
Msingi wa kesi hiyo unaosimamiwa na mawakili wa upande wa ulalamikaji wa Rex ni kuiomba Mahakama hiyo itangaze kuwa sheria iliyopitishwa na Bunge ya kila mtumiaji wa simu ya mkononi kukatwa Sh 1,000 kwa mwezi ni kandamizi.
Aidha, wanataka Mahakama hiyo imzuie Waziri wa Fedha kupitia TRA kutoza kodi hiyo hadi maombi yao yatakapotolewa uamuzi. Pamoja na TRA kukiri kutoa agizo la kuanza kukatwa kwa kodi hiyo na kutofafanua, kuna taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku (si HabariLeo) kuwa waraka huo umezitaka kampuni hizo kuanza kutoza kodi hiyo ya Julai, Agosti na Septemba na kuendelea.
Tangu kupitishwa kwa kodi hiyo na Bunge, Aprili mwaka huu, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, wanasiasa na wanaharakati ya kuipinga kwa kuwa itafanya wananchi wengi wenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama za kumiliki simu.
Malalamiko hayo, yalimlazimu Rais Jakaya Kikwete kukutana na wadau wa mawasiliano ambao ni wamiliki wa Kampuni za Simu Tanzania (MOAT), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kisha kuwaagiza wakae na kufikiria mbadala wa kodi hiyo kama itaondolewa, jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.
Kampuni hizo za simu zikitekeleza agizo la waraka huo mwezi jana, takribani wateja milioni nane wa simu watakatwa Sh 3,000 ili kufidia kodi ya simu ya Sh 1,000 kwa kila mwezi kuanzia Julai kodi hiyo ilipotakiwa kuanza kutozwa kisheria kwa kila mtumiaji simu.

No comments:

Post a Comment

Adbox

@templatesyard