MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA)
imekiri kuziandikia waraka kampuni za simu nchini kuzitaka zianze kukata
kodi mpya ya laini mara moja kuanzia mwezi huu. Kodi hiyo mpya
ilipitishwa wakati wa Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 na
kutaka utekelezaji wake uanze Julai 30, ili kusaidia shughuli za bajeti
ya Serikali Kuu.
Akijibu swali kuhusu ukweli wa Mamlaka
hiyo kuagiza kampuni hizo kuanza rasmi kutoza kodi hiyo mwezi jana,
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mteja, Huduma na Mapato wa TRA, Richard Kayombo,
alikiri kutoa agizo hilo.
“Sitaki kuzungumzia kiundani sana suala
hili, lakini ukweli ni kwamba kampuni hizi za simu zimeandikiwa kuanza
kulipa kodi na tumeandika kwa ajili ya utekelezaji wa kodi hii mpya,”
alisema Kayombo.
Alisema ingawa kweli kampuni hizo
zimeagizwa kuanza kutoza kodi hiyo, hatazungumzia zaidi suala hilo kwa
kuwa tayari liko mahakamani hivyo si vema kuingilia uhuru wa mhimili
huo. Wakati TRA ikitoa agizo hilo, Taasisi ya Watumiaji wa Bidhaa na
Huduma ilifungua kesi Mahakama Kuu kupinga sheria hiyo.
Taasisi hiyo ilifungua kesi hiyo hivi
karibuni katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya
dharura na kuanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni
Lawrence Kaduri, Aloysius Mujulizi na Salvatory Bongole.
Msingi wa kesi hiyo unaosimamiwa na
mawakili wa upande wa ulalamikaji wa Rex ni kuiomba Mahakama hiyo
itangaze kuwa sheria iliyopitishwa na Bunge ya kila mtumiaji wa simu ya
mkononi kukatwa Sh 1,000 kwa mwezi ni kandamizi.
Aidha, wanataka Mahakama hiyo imzuie
Waziri wa Fedha kupitia TRA kutoza kodi hiyo hadi maombi yao
yatakapotolewa uamuzi. Pamoja na TRA kukiri kutoa agizo la kuanza
kukatwa kwa kodi hiyo na kutofafanua, kuna taarifa zilizoandikwa na
gazeti moja la kila siku (si HabariLeo) kuwa waraka huo umezitaka
kampuni hizo kuanza kutoza kodi hiyo ya Julai, Agosti na Septemba na
kuendelea.
Tangu kupitishwa kwa kodi hiyo na
Bunge, Aprili mwaka huu, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi, wanasiasa na wanaharakati ya kuipinga kwa kuwa itafanya
wananchi wengi wenye kipato kidogo kushindwa kumudu gharama za kumiliki
simu.
Malalamiko hayo, yalimlazimu Rais
Jakaya Kikwete kukutana na wadau wa mawasiliano ambao ni wamiliki wa
Kampuni za Simu Tanzania (MOAT), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kisha
kuwaagiza wakae na kufikiria mbadala wa kodi hiyo kama itaondolewa,
jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.
Kampuni hizo za simu zikitekeleza agizo
la waraka huo mwezi jana, takribani wateja milioni nane wa simu
watakatwa Sh 3,000 ili kufidia kodi ya simu ya Sh 1,000 kwa kila mwezi
kuanzia Julai kodi hiyo ilipotakiwa kuanza kutozwa kisheria kwa kila
mtumiaji simu.
No comments:
Post a Comment