YANGA YATOA TAARIFA KUHUSU UWANJA WAO WA KISASA!!

                                                                                                                                                                    
 YANGA_MJENGO

             LEO tungependa kupitia kwenu kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi wetu wa Uwanja wa kisasa wa mpira katika Jiji la Jangwani kama itakavyojulikana
Mara ya mwisho tuliongea ama kuonana ilikuwa mwezi wa tatu wakati Ndugu zetu wa BCEG walipokabizi Concept design ama Usanifu wa awali na kuanzia sasa tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mradi huu. Wahenga walisema UKICHA KUSEMA HUTATENDA JAMBO lakini pia KUKAA KIMYA SANA kunajenga hisia mbaya na kutoa nafasi ya upotoshwaji wa habari.
Kwa kifupi napenda kuwakumbusha kuwa Makubalino ya Awali (Memorandum of Understanding) yalisainiwa 23 Novemba 2012. Pamoja na mengineyo YANGA inatakiwa:
•        Kupata na kuwa na eneo la kutoshereza malengo ya mradi
•        Kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi
•        Kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi
Kwa upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa kutosha. BCEG wameandaa na kukabidhi michoro ya usanifu wa awali kukidhi matakwa ya YANGA. YANGA tunatakiwa kutoa maoni yetu na na kuingia RASMI mkataba wa ujenzi.
Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es Salaam, na katika hali ya kutaka klabu iwe na vitega uchumi klabu imeonelea ni vyema kama ingekuwa na uwanja wa mpira wa karne ya sasa na baadaye ambao pamoja na mambo mengine utakuwa na mioundombinu ifuatayo:-
1. Uwanja wa mpira wenye viti 40,000
2. Hostel ya wachezaji na football academy ya vijana
3. Viwanja vya mazoezi
4. Uwanja wa kutosha kuegesha magari
5. Hoteli na sehemu ya makazi
6. Ukumbi wa mikutano
7. Sehemu ya maofisi, benki, zahanati (sports clinic)
8. Maduka, supermarket na sinema
9. Sehemu za kubarizi, kupumzikia (Recretional and Open spaces)
Mara baada ya azma yetu kukamilika eneo hili litaitwa “Jangwani City” na kufanya wakazi wa maeneo ya Jangwani na sehemu za jirani wasiende maeneo ya mbali kutafuta huduma muhimu za kijamii. Eneo hili litaboresha mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza mazingira na miundombinu. Hii itahusu pamoja na mambo mengine ujazaji udongo (tuta kubwa), upandaji miti, bustani za kubarizi, kuboresha mifereji ya majitaka na kudhibiti mafuriko ya eneo la Jangwani na hivyo kulipatia sura ya kibiashara na kitalii.
Ili kukamilisha azma ya kuwa na Jangwani City itakayo kuwa na miundombinu yote hiyo, Uongozi ulipeleka maombi ya eneo la nyongeza Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa barua zenye kumbukumbu namba YASC/ARDHI/MWK/YM/46/2012 na YASC/ARDHI/MWK/YM/47/2012 za 12 Desemba 2012, na mpaka sasa bado maombi yetu hayajajibiwa.
Mwezi wa saba, Wadhamini/Uongozi wa YANGA walimwandikia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada wake kufanikisha maombi ya nyongeza ya kiwanja yaliyowasilishwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Klabu ya Yanga ina kiwanja chenye ukubwa wa hekta 3.59 eneo la Jangwani. Kiwanja hiki kina hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na katika eneo hilo, klabu ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na Jengo la klabu la ghorofa tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili mkubwa sana wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) na michango ya wanachama na wapenzi wa klabu ambao kila siku wamekuwa wakiamini kuwa haba na haba hujaza kibaba.
Ndugu Wandishi wa habari kwa kifupi tumefikia hapo, zoezi la kutoa maoni yetu kuhusu michoro ya usanifu wa awali na kuingia rasmi mkataba wa ujenzi na BCEG limesimama, likisubiri majibu ya nyongeza la eneo.  Ni matumaini yetu zoezi hili litakamilika hivi karibuni na kuendelea na mradi.
YANGA_MJENGO

No comments:

Post a Comment

Adbox

@templatesyard