RAHA NI ARSENAL v NAPOLI, STEAU v CHELSEA, PORTO v ATLETICO, CELTIC v BARCA!
MECHI za Pili za Makundi E hadi H zipo
Dimbani leo huku Chelsea wakiwa Ugenini wakisaka ushindi wao wa kwanza
baada ya kutandikwa katika Mechi yao ya kwanza, Arsenal wapo Emirates na
mtanange mkali sana na Napoli huku Vigogo Barcelona, bila ya Supastaa
Lionel Messi, wakiwa Ugenini Uwanja wa Celtic Park ambako Msimu uliopita
walinyukwa.
PATA TAARIFA ZAIDI:
RATIBA:
[Saa za Bongo]
Jumanne 1 Oktoba 2013
[Saa 1 Usiku]
Football Club Zenit v FK Austria Wien
[Zote kuanza Saa 3 Dakika 45 Usiku]
FC Basel 1893 v FC Schalke 04
FC Steaua Bucureşti v Chelsea FC
Borussia Dortmund v Olympique de Marseille
Arsenal FC v SSC Napoli
FC Porto Club v Atlético de Madrid
AFC Ajax v AC Milan
Celtic FC v FC Barcelona
KUNDI E
Basle v Schalke
Basle, ambao walifika Nusu Fainali ya
EUROPA LIGI Msimu uliopita, wameanza Kundi hili kwa kishindo kwa
kuitwanga Chelsea 2-1 huko Stamford Bridge kwa Bao za Mohamed Salah na
Marco Streller na huo ukawa ushindi wa kwanza kwa Klabu za Uswisi Nchini
England katika Mechi 20.
Mara ya mwisho Basel kukutana na Klabu ya
Germany ni kwenye Raundi ya Mtoano ya Timu 16 za UCL Msimu wa 2011/12
na kuchapwa 7-0 na Bayern Munich.
Basel ndio wanaongoza Ligi ya Uswisi lakini kwenye Mechi yao ya mwisho walitoka Sare 2-2 na Sion.
Schalke walishinda Mechi yao ya kwanza ya
Kundi hili kwa kuichapa Steaua Bucharest 3-0 lakini kwenye Bundesliga
wapo katikati kwenye Msimamo na Jumamosi iliyopita waliongoza 2-0 dhidi
ya Hoffenheim na kulazimishwa Sare ya 3-3.
Kevin-Prince Boateng, Nyota wao walipoifunga Steaua Bucharest, Jumamosi alifunga Bao.
Steaua Bucharest v Chelsea
Chelsea wamejitayarisha kwa Mechi hii kwa
Jumamosi kutoka Sare ya 1-1 na Tottenham huku Straika wao Fernando
Torres akitolewa nje kwa Kadi Nyekundu.
Hii ni Mechi ambayo hata Kocha wa Chelsea
Jose Mourinho amekiri hawatakiwi kuipoteza kwa vile walichapwa 2-1 na
FC Basel katika Mechi ya kwanza ya Kundi hili.
Msimu uliopita Steaua iliifunga Chelsea
1-0 kwenye Raundi ya Mtoano ya EUROPA LIGI lakini wakachapwa 3-1 kwenye
Marudiano huko Stamford Bridge.
KUNDI F
Arsenal v Napoli
Arsenal waliuanza Msimu huu kwa kuchapwa
3-1 na Aston Villa kwenye Ligi Kuu England lakini tangu hapo wameshinda
Mechi 9 mfululizo na sasa wanaongoza Ligi hiyo na ushindi huo ni pamoja
na kuifunga Ugenini Marseille Bao 2-1 kwenye Mechi ya kwanza ya Kundi
hili.
Wikiendi hii iliyopita, Arsenal
waliifunga Swansea City Bao 2-1 kwenye Ligi huku Kiungo wao Aaron Ramsey
akifunga Bao na hiyo ni Gemu 4 mfululizo anapachika Mabao.
Rafael Benitez, aliewahi kuwa Meneja wa
Liverpool na Chelsea, ndie aiongoza Napoli ambayo kwenye Serie A huko
Italy inafanya vyema sana wakiwa wametoka Sare Mechi moja tu kati ya 6
walizocheza na wako Nafasi ya Pili, Pointi 2 nyuma ya Vinara AS Roma.
Jana Napoli walitangaza Kikosi chao ambacho kimetua London kuikabili Arsenal na nacho ni:
Makipa: Rafael, Reina, Colombo.
Mabeki: Albiol, Britos, Cannavaro, Fernandez.
Viungo: Armero, Behrami, Dzemaili, Hamsik, Inler, Mesto, Radosevic, Zuniga.
Mafowadi: Callejon, Mertens, Higuain, Insigne, Pandev, Duvan.
Borussia Dortmund v Marseille
Borussia Dortmund, ambao walifika Fainali
ya Mashindano haya Msimu uliopita, wameanza vyema Bundesliga na
kuongoza kwa kushinda Mechi 6 kati ya 7 na Jumamosi waliishindilia
Freiburg Bao 5-0.
Lakini kwenye UCL kwenye Kundi hili
wameanza vibaya kwa kufungwa 2-1 Ugenini na Napoli katika Mechi ambayo
Kipa wao Roman Weidenfeller alitolewa kwa Kadi Nyekundu, hivyo hachezi
Mechi hii, na pia Kocha wao Jurgen Klopp, kutolewa nje na Refa.
KUNDI G
Zenit Saint Petersbug v Austria Vienna
Timu zote hizi zimefungwa Mechi zao za
kwanza kwa Zenit kufungwa Ugenini 3-0 na Atletico Madrid na Vienna
kuchapwa Nyumbani kwao 1-0 na FC Porto.
Lakini Zenit, wakicheza Nyumbani ni
wakali na ambako ndio wanaongoza Ligi ya Urusi na Juzi kuwafunga Spartak
Moscow 4-2 huku Alexander Kerzhakov akipiga Bao lake la 208 kwenye Ligi
na kumfanya awe Mfungaji Bora katika Historia ya Ligi ya Urusi.
Austria Vienna wapo Nafasi ya 5 kwenye Ligi ya kwao na walifungwa 1-0 na Admira hivi Juzi.
FC Porto v Atletico Madrid
Atletico Madrid wako moto huko kwao
kwenye La Liga kwa kukamatana Pointi sawa na Vinara Barcelona na Juzi
waliichapa Real Madrid 1-0, kwa Bao la Mbrazil Diego Costa, huko
Santiago Bernabeu na kuua Rekodi ya kutoifunga Real kwenye Ligi kwa
Miaka 14.
Hata hivyo, Atletico watatinga Mechi hii bila Diego Costa ambae anamalizia Kifungo chake cha Mechi za Ulaya 4.
Porto nao wanaongoza Ligi yao wakiwa Pointi 2 mbelle ya Sporting Lisbon huku kila Timu ikiwa imecheza Mechi 6.
KUNDI H
Ajax v AC Milan
Ajax wapo Nyumbani na katika Mechi ya kwanza ya Kundi hili walichapwa 4-0 Ugenini na Barcelona.
Ajax wamejitayarisha kwa Mechi hii kwa
kuidunda Go Ahead Eagles Bao 6-0 kwenye Mechi ya Ligi ya kwao na
kuwafanya wawe Pointi 1 nyuma ya Vinara PSV Eindhoven.
Nao AC Milan, ambao wameshinda Mechi 2 tu
za Serie A kati ya 6 na wapo Nafasi ya 9, wanatinga kwenye Mechi hii
wakiwa na Majeruhi kadhaa lakini walishinda Mechi yao ya kwanza ya Kundi
kwa kuichapa Celtic 2-0.
Celtic v Barcelona
Msimu uliopita kwenye Hatua ya Makundi ya
UCL, Celtic waliichapa Barcelona 2-1 ndani ya Celtic Park na leo
Barcelona wanatinga tena bila ya Supastaa wao Lionel Messi ambae ni
Majeruhi baada kuumia Jumamosi iliyopita kwenye Mechi ya La Liga
walipoichapa Almeria 2-0.
RATIBA:
[Saa za Bongo]
Jumatano 2 Oktoba 2013
[Saa 1 Usiku]
PFC CSKA Moskva v FC Viktoria Plzeň
[Zote kuanza Saa 3 Dakika 45 Usiku]
FC Shakhtar Donetsk v Manchester United FC
Bayer 04 Leverkusen v Real Sociedad de Fútbol
Juventus v Galatasaray A.Ş.
Real Madrid CF FC København
Paris Saint-Germain v SL Benfica
RSC Anderlecht v Olympiacos FC
Manchester City FC v FC Bayern München
No comments:
Post a Comment