HUKUMU YA MASOGANGE.. MCHEZO UMECHEZWA!

“Hivi jamani, hiki sasa ni kiini macho. Tuliambiwa lakini watatoka tu. Mamlaka ya mapato kule Sauzi waliona ni madawa ya kulevya, mahakama ikaona ni kemikali hatari, mnadhani nani mkweli hapo?”

Stori:  Waandishi Wetu
VIDEO Queen wa Bongo, Agnes Gerald Waya ‘Masogange’ na shosti yake, Melissa Edward wapo huru kufuatia kesi iliyokuwa ikisikilizwa nchini Afrika Kusini ya kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya Crystal Methamphetamine ya Sh. bilioni 6.8, lakini baadhi ya wadau nchini wanasema kuna mchezo umechezwa, Ijumaa Wikienda limebaini mambo ya kushangaza nyuma ya pazia. 
Masogange na Melissa walikamatwa Julai 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo Kempton Park jijini Johannesburg nchini humo. Wawili hao wameishi mahabusu kwa saa 1824.

MMOJA HURU, MMOJA AHUKUMIWA
Uhuru wa Masogange ni baada ya Mahakama ya Kempton jijini Johannesburg kumtia hatiani kwa kuingiza kemikali hatari nchini humo, akatakiwa kulipa faini ya randi 30,000 (Sh. milioni 4.8 za Bongo) au kifungo cha miaka 2 jela.
Melissa yeye hakukutwa na hatia kwa vile ilibainika mizigo aliyokutwa nayo aliombwa na Masogange amsaidie kubeba baada ya kukutana ndani ya ndege ya Shirika la South Africa Airlines.

KUMBE SI CRYSTAL MATHAMPHETAMINE
Habari kutoka nchini humo zinasema mdhamini wa Masogange (jina halijapatikana) alipigana kuhakikisha staa huyo na nduguye ambaye amezaliwa naye kwa mama mkubwa wanakuwa huru na kurejea Bongo.
Katika kupigana huko, mdhamini huyo alifurahia matokeo ya uchunguzi wa mkemia mkuu wa serikali ya nchi hiyo kuyaona madawa hayo kuwa si Crystal Methamphetamine bali ni Ephedrine ambayo si unga ila ni kemikali hatari ambayo ikichanganywa na dawa nyingine hupatikana unga halisi.
Kwa Bongo madawa hayohayo ni unga na tayari watu wengi wapo korokoroni kwa kukamatwa nayo akiwemo aliyekuwa rafiki wa marehemu Steven Kanumba, Saada Ally.
Katika hilo, mtu anayekamatwa na madawa hayo nchini humo hushtakiwa kwa kosa la kuingiza kemikali hatari. Serikali ya Afrika Kusini ilipiga marufuku kuingizwa nchini humo kwa madawa hayo na adhabu yake iko wazi.
“Yule mdhamini alipojua mkemia mkuu amesema yale si Crystal Methamphetamine bali ni Ephedrine aliitumia nafasi hiyo kucheza na mwanasheria ambapo kifungo chake kinajulikana,” alisema mtoa habari wetu mmoja.

MSEMAJI WA ‘TRA’ YA SAUZ AINGIA SHAKA
Habari zinasema kuwa, kufuatia taarifa za mahakama kwamba mzigo huo si Crystal Methamphetamine bali ni Ephedrine Msemaji wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini (SARS), Marika Muller alisema kuwa timu yake ina uhakika wa asilimia mia moja kwamba, mzigo wote wa Masogange na Melissa walioukamatwa  nao ni madawa ya kulevya aina ya Crystal Meth.
Muller akatoa la moyoni akisema kwamba, kama mahakama imekubaliana na matokeo ya uchunguzi wa mkemia mkuu wa nchi hiyo, yeye hana la kusema kwa kuwa uamuzi wa korti ni wa mwisho.

KAMANDA NZOWA ANYOOSHA MIKONO
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa ambapo alipoulizwa juzi kama serikali ina mpango wa kumkamata Masogange atakaporejea nchini ili awataje waliomtuma, alisema:
“Sasa kama wameachiwa kule, sisi tutawakamataje? Hatuna sababu ya kufanya hivyo, kesi ilisikilizwa kule mahakama ikafikia ilipofikia, basi tena! Ila tutafuatilia chini kwa chini mtandao huo.”


MCHEZO UMECHEZWA 
Jijini Dar es Salaam, baadhi ya wasomaji walipozungumza na gazeti hili juzi walitilia shaka kuwepo kwa mazingira ya kuchakachuliwa kwa madawa hayo.
Walisema kuwa, ilikuwaje SARS iwakamate akina Masogange na kugundua walibeba Crystal Meth (unga) halafu mahakama iseme ni Ephedrine (kemikali hatari)?
“Hivi jamani, hiki sasa ni kiini macho. Tuliambiwa lakini watatoka tu. Mamlaka ya mapato kule Sauzi waliona ni madawa ya kulevya, mahakama ikaona ni kemikali hatari, mnadhani nani mkweli hapo?” alihoji msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Aunt Elizabeth, mkazi wa Mbezi Beach, Dar.
Wengine walitupia kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na Twitter wakidai hivyohivyo kwamba kuna mchezo umechezwa.
“Kwanza wamekamatwa Julai 5, mwaka huu. Kesi imeisha katikati ya wiki iliyopita, hata miezi mitatu haikufika. Hapa Bongo, yule mama Leila (Mwanaidi Mfundo) na wenzake walikamatwa 2011 kwa unga huohuo, kesi yao bado ipo Mahakama Kuu, Dar hadi leo,” alisema Samuel Msalanda wa Ilala, Dar.
Wengi walionesha kutilia shaka hukumu hiyo kutokana na mitazamo yao lakini Mahakama ya Kempton jijini Johannesburg, Afrika Kusini ndivyo ilivyoamua.

MASWALI TATA  
Ukiachana na mitazamo na ukweli ulivyo, bado kuna maswali tata ambayo utatuzi wake unakuwa mgumu kulingana na kesi yenyewe kuanzia kutajwa, kusikilizwa hadi hukumu ilikuwa nje ya Tanzania.
Je, mwenyewe Masogange alipokuwa akisafirisha dawa hizo alijua ni kemikali hatari ambayo ni mali ghafi ya madawa ya kulevya?
Iwe ni kemikali au la! Alitoa wapi mali ghafi hiyo na alikuwa akimpelekea nani kule Afrika Kusini?
Ni kigogo au mtu gani aliyeratibu safari hiyo mpaka Masogange akafanikiwa kupita kwenda Afrika Kusini?
Nani alimpeleka Masogange hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)?
Kituo cha kwanza cha Masogange kuondokea kwenda JNIA kilikuwa wapi? Inawezekana ni nyumbani kwake ambapo alilala na mizigo yote ile?
Kama mahakama imebaini Masogange hakuingia Afrika Kusini  na unga, vipi kuhusu wale  wafanyakazi wa  JNIA walioachishwa kazi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kwa kuzembea Masogange akapita na ule mzigo?
Yupo wapi Nassoro Mangunga aliyetajwa na Dk. Mwakyembe kuwa alifanikiwa kutoroka na mabegi matatu ya unga kule Sauzi?

No comments:

Post a Comment

Adbox

@templatesyard